David Kafulila apangua hoja zote za Zitto Kabwe kuhusu ripoti ya CAG
1.
Baada ya Chama Cha ACT kutoa tamko lao kwa kina Jana kuhusu Ripoti ya
CAG kwa hesabu za 2016/17, nimeulizwa na wadau wengi kuhusu maoni yangu
kufuatia tamko hilo wakihusianisha na msimamo wangu kwamba serikali ya
awamu ya tano ni tofauti sana na hivyo kutaka kunisikia maoni yangu
kufuatia kilichoitwa madudu yaliyobainishwa katika uchambuzi wa chama
cha ACT kuhusu serikali hii kwa mujibu wa ripoti hiyo.
Kwanza
niwapongeze ACT kwa kuunguza bongo hata kutoka na tamko
lililosababisha mjadala wa masuala muhimu kwa Taifa. Binafsi naamini
kwamba Ripoti za CAG ni kioo kwa Serikali na Mamlaka zake,nakwasasa ni
kioo kwa vyama vya siasa pia, ndio sababu serikali huzipa uzito wa
kipekee kwa kuchukua hatua haraka na hivyo kutoa somo kwa vyama vya
siasa kufanya hivyo pia.Hivyo nawapongeza ACT kuipa joto hoja ya CAG ili
tujadili na kubadilishana mawazo kwa maslahi ya Taifa.
Katika
hoja ya 7, ACT wanasema ” Kwa ujumla Serikali imepata hati
Chafu.Taarifa ya CAG ya ukaguzi wa kwanza wa makusanyo na matumizi ya
kibajeti ya Serikali ya awamu ya tano, imeonesha kuwa , kwa ujumla ,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano imepata hati Chafu , kwakuwa Hesabu
Jumuifu za Taifa ( Consolidated Accounts ) zimepata Hati ISIYORIDHISHA (
Chafu).”
UKWELI
nikwamba Nimesoma Ripoti hiyo yenye kurasa 434, sikukuta mahala CAG
ameandika kwa kigezo chochote kwamba Serikali kwa ujumla imepata hati
Chafu.Nikajaribu kusoma mijadala kutafuta nani ameweza kutoa Rejea ya ni
wapi CAG kasema hilo, nikakuta kwenye mjadala wa Jamiiforum, Kiongozi
Mkuu wa ACT amemjibu mmoja wa waliotaka kujua ni wapi CAG kasema kwa
ujumla Serikali imepata hati Chafu, katibu majibu yake, Kiongozi huyo
katika majibu yake kwenye mjadala huo muda(8:09PM) ameandika kwamba CAG
amesema hilo kwenye ukurasa wa
298.
NIMERUDIA KUSOMA UKURASA HUO NENO KWA NENO HAKUNA KITU HICHO. Ukurasa
huo umeleza mapungufu ya hesabu, lakini hakuna maneno ambayo ACT inataka
kuaminisha Umma kuwa yametajwa na CAG.
Inawezekana
ACT baada ya kusoma maelezo hayo wakahitimisha kwamba Serikali kwa
ujumla imepata hati Chafu.Hata hivyo, Mwenye Mamlaka ya kuamua madaraja
ya Hati si Mwingine bali CAG kwa kuzingatia viwango vya Kimataifa vya
Ukaguzi wa Taasisi za Umma( ISSAIs) na Bodi ya Kimataifa ya Maadili kwa
kanuni za Maadili ya wahasibu ( Kanuni ya IESBA). Hivyo sio mtu yeyote
au chama au taasisi inamamlaka ya kusoma hesabu na kuzipangia daraja la
Hati kama ACT wanavyotaka kufanya. Ni kwa msingi huo maneno kwamba
Serikali imepata hati Chafu yanabaki kuwa kwa mujibu wa chama cha ACT na
sio CAG .
2.
Kwenye hoja 1, ACT wanasema Mawaziri wanafanya makosa kujibu hoja za
CAG kwa waandishi wa habari na kwamba sheria ya Ukaguzi wa Umma
kifungu38(1)&(2) kinaeleza Maafisa Masuuli/ Makatibu Wakuu ndio
wanapaswa kujibu hoja zilizoibuliwa na CAG tena mbele ya Kamati ya
PAC&LAAC.
UKWELI
Nikwamba Mawaziri wangejibu hoja za CAG mbele ya Kamati za PAC&
LAAC wangekuwa wamevunja Sheria hiyo, lakini Mawaziri kueleza Waandishi
wa Habari maoni yao au hatua wamezokwisha kuchukua kuhusu Ripoti ya CAG
haijakatazwa popote kwenye sheria hiyo kwani wanahabari sio kamati ya
PAC wala LAAC kama ilivyotajwa katika sheria hiyo.Ndio sababu tamko hilo
hilo la ACT, pamoja na kujua kwamba Ripoti hiyo haijaanza kufanyiwa
kazi na Kamati za PAC& LAAC , ACT wamepongeza Serikali kuanza
kuchukua hatua hadharani kufuatia Ripoti hiyo. Hivyo walichokipongeza
ndicho wanachokihoji tena kwenye tamko hilo hilo.
3.Kuhusu
kinachoitwa upotevu wa 1.5trilioni. Kwa mujibu wa ACT nikwamba kwakuwa
kwenye ukaguzi wa matumizi imeonekana kiasi kilichotolewa ni trilioni
23.8..wakati kwenye makusanyo kilichopatikana ni trilioni 25.3 .hivyo
kuna upotevu wa 1.5trilioni.
UKWELI
ni kwamba kwamba ACT ilipaswa kuweka hoja hii katika mfumo wa swali
badala ya kuhitimisha kwani hata CAG hakuna mahala amehitimisha kuwa
kuna upotevu wa trilioni1.5. Nasema walipaswa kuuliza kwasababu Mimi
baada ya kusoma Hotuba ya Bajeti 2017/18, kwenye eneo la Mapitio ya
Bajeti ya 2016/17 ambayo ndio hesabu zake zimekaguliwa, Waziri wa Fedha
kwenye Hotuba yake alibainisha wazi kwenye Paragrafu ya 2 kipengele cha
mapitio ya matumizi kwamba Kati ya Pesa za miradi ya maendeleo kutoka
nje( trilioni trilioni 3.047).Kuna kiasi cha Pesa hizo Matumizi yake
hayakupitia mfumo wa malipo wa Serikali baada ya baadhi ya washirika wa
maendeleo kuzipeleka moja kwa moja kwenye miradi.
Nanukuuu
” Hata hivyo ,baadhi ya fedha za nje za kugharimia miradi ya Maendeleo
hazikujumuishwa kwenye matumizi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo
kuchelewa kupata thamani halisi ya vifaa vilivyopelekwa moja kwa moja
kwenye miradi kutokana na baadhi ya washirika wa Maendeleo kuendelea
kupeleka fedha moja kwa moja bila kupitia mfumo wa malipo wa Serikali”
Katika
msingi huo ni wazi fedha ambazo hazikutolewa kupitia mfumo wa malipo wa
Serikali CAG asingeweza kuziona na hivyo kujitokeza kwa tofauti ya
makusanyo na fedha iliyolipwa sio jambo la kushangaza katika mazingira
hayo.Najua Serikali inaweza kueleza hili kwa takwimu zaidi.
4.
Hoja kwamba Serikali imetekeleza Bajeti kwa asilimia 68% huku Bajeti ya
Serikali za mitaa ikitekelezwa kwa asilimia 51ni utekelezaji hafifu
nadhani ingekuwa vema kama ACT wangefanya ulinganisho.waseme kiasi hicho
ni kidogo kulinganisha na miaka gani. Kwani navyojua miaka michache
iliyopita Bajeti ya Serikali za mitaa ilitekelezwa mpaka kwa
asilimia35%.
Hivyo utekelezaji huu wa asilimia 51 % ni hatua kubwa hata kama haitoshi kwakuwa haijafika asilimia100%.
5.
Kwamba ACT wanasema Madeni ya nyuma yaliyolipwa bila idhini ya bunge
ni madeni hewa, Nadhani ACT wangetafuta msamiati tofauti kwani madeni
hewa ni Yale yasiyokuwepo, lakini kama yamehakikiwa kuwa ni madeni
halali hayawezi kuitwa madeni hewa.
6.
Kwamba CAG hakukagua ATCL hivyo nikasoro kwa CAG, nadhani ibaki kama
walivyoshauri kwamba ukaguzi ujao CAG aone haja ya kukagua lakini huwezi
kumlaumu kutokagua kwa hoja tu manunuzi ya ndege yalifanyika katika
mwaka huo wa fedha uliokaguliwa 2016/17 kwani hakuna mwaka CAG alikagua
mashirika yote. laiti ingekuwa yamekaguliwa mashirika yote likaachwa
ATCL kulikuwa na uhalali wa kuhoji kulikoni.
7.
Hoja kwamba Matumizi ya Serikali yanapangwa na Ikulu siku hizi badala
ya Serikali ni tuhuma nzito, ingawa kwakuwa wameitoa bila uthibitisho
wowote ni ngumu kwa mtu makini kuipa uzito sawia na hivyo inakosa uzito
na kuonekana kama vijembe vya kisiasa tu.
8.
Hoja kwamba namna serikali inavyokopa ndani kupitia minada ya dhamana
za Serikali inasababisha Benki za biashara kuvutiwa zaidi kuikopesha
serikali badala ya sekta binafsi na hivyo kufanya biashara isichangamke
ni hoja inayohitaji mjadala mpana.
Nasema
hivyo kwasababu kwenye awamu ya nne tulilalamika kwamba Serikali
ilikuwa inakopa ndani kwa mfumo huo lakini kwa riba juu sana mpaka
zaidi ya asilimia17% mwaka 2015 kwa TBs za Sik182&365 na hivyo hoja
ikawa ni kwamba Benki zinapoteza hamu ya kukopesha sekta binafsi na
hata kuongeza riba zaidi kwa kulinganisha na riba ambayo Benki huvuna
inapoikopesha serikali( kwasababu Benki zinajua Serikali ni Risk free).
Ni
kwasababu hiyo tukawa tunajenga hoja bungeni serikali isikope kwa riba
ya juu katika masoko ya dhamana ili Benki za biashara ziwe na hamu ya
kukopesha sekta binafsi na kwa riba nafuu.
Kitu
ambacho Serikali hii imetekeleza, kwamba kwasasa Serikali inakopa
kwenye mfumo huo wa TBs kwa riba ya asilimia 5% kwa TBs za siku365 na
riba ya kwa TBs za siku182.Hii inathibitisha wazi dhamira ya serikali
kutozivutia Benki za biashara ziikopeshe n badala yake zijielekeze
kwenye sekta binafsi kwani riba zinayopata sasa kwa kuikopesha Serikali
ni pungufu kwa zaidi ya asilimia 300% kulinganisha na mwaka 2015.
9.
Mwisho nihitimishe kwa kuipongeza Serikali kwa namna imevyofanikiwa
kutekeleza kilichokuwa kilio cha Bunge la 9&10 kuhusu misamaha ya
kodi ambapo kwa miaka10 mabunge hayo yalipigania misamaha ishuke mpaka
asilimia1% ya pato la Taifa ikitolewa mifano ya nchi wanachama Afrika
Mashariki kama kigezo( misamaha yake ilikuwa asilimia1% ya Pato la
Taifa). Miaka miwili yote ya Serikali hii, misamaha ya kodi ni
asilimia1% kutoka asilimia2 % mpaka asilimia3% ya pato la Taifa kabla ya
awamu hii( Kwa mujibu wa Ripoti hii ya CAG).
Aidha
ufanisi wa TRA katika kukusanya kodi tangu mwaka 2016 upo juu kuliko
miaka mingi kama inavyojieleza kwenye Ripoti ya CAG ukurasa wa
31&32. Ambapo imebainishwa kwamfano, mwaka 2013/14 makadirio ya
makusanyo ya kodi yalikuwa billion10,320 lakini ikakusanywa bilioni
9289 , sawa na pungufu ya bilioni 1031, Mwaka 2014/15 Makisio ilikuwa
kukusanya billion11262 lakini ikakusanywa billion9919 sawa na pungufu ya
billioni1343. Lakini Mwaka wa Kwanza wa awamu ya tano, hesabu za
2015/16 , Makadirio yalikuwa billioni12363 lakini makusanyo yakafika
billion12464 sawa na ziada ya billion101 na hata mwaka 2016/17 ambapo
makisio yalikuwa juu kuliko mwenendo wa awali kwa kuwekwa billioni 15105
lakini bado makusanyo yalifika billioni14271 sawa na pungufu ya
billioni834,pungufu ambayo bado ni kidogo kulinganisha na miaka
iliyotangulia.( Rejea Ripoti ya CAG ukurasa31&32).
Niwashukuru watanzania wote mliohitaji kusikia maoni yangu.
David KAFULILA
Leo Aprili16,2018.

No comments: