Wadau washauri soko la pamoja la dhahabu
WADAU wa sekta ya madini wamependekeza kuanzisha soko la pamoja la dhahabu nchini. Wamesema soko hilo litasaidia kudhibiti utoroshaji wa madini hayo, lakini pia kuhakikisha sekta ya madini inaongeza mchango wake katika pato la taifa.
Kauli hiyo ilitamkwa mwishoni mwa wiki wakati wa mkutano wa wadau wa madini katika mikoa ya Kanda ya Ziwa uliojadili namna ya kuongeza pato la taifa kupitia sekta ya madini, huku Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akiwa miongoni mwa washiriki.
Waliazimia kwa sauti moja kudhibiti utoroshaji wa madini ili kuongeza mchango wake katika uchumi wa nchi. Kutokana na maazimio hayo, mkutano uliunda Kamati yenye wajumbe 14 kutoka kada mbalimbali za sekta husika, Mwenyekiti ambaye ni Rais wa sasa wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), John Bina na Katibu ambaye ni Kamishna Msaidizi wa Madini, Kanda ya Ziwa Viktoria – Magharibi, Yahya Samamba.
Akiwasilisha hadidu za rejea kwa Kamati husika ambayo imeahidi kukamilisha kazi iliyopewa ndani ya siku 30 kuanzia juzi Februari 25, Mwenyekiti wa mkutano ambaye ni Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, alizitaja kuwa ni pamoja na kuainisha utaratibu utakaotumika kuanzisha soko hilo la dhahabu katika Jiji la Mwanza kama ilivyopendekezwa.
Ametaja kazi nyingine inayopaswa kufanywa na kamati hiyo kuwa ni kubainisha mbinu zitakazotumika kupata washiriki wa mnada huo, ikiwa ni pamoja na wauzaji na wanunuzi.
Aidha, alisema kamati husika itatakiwa kuainisha miundombinu ya mnada mzima kwa maana ya mpangilio wa wote watakaohusika katika mnada huo kama vile watu wa kodi, benki mbalimbali na wengineo.
“Kwa ufupi watapaswa kuainisha shughuli zote ambazo zitaendana na mnada zifanyike vipi,” alisema.
Kamati pia imetakiwa kuandaa na kuwasilisha mkakati utakaobainisha utaratibu mzima au mbinu sahihi zinazopaswa kutumika kuanzia ununuzi hadi upatikanaji wa kibali cha kusafirisha madini nje ya nchi kwa kutumia muda mfupi. Kazi nyingine ya kamati husika ni kupambanua faida na hasara za uwepo wa soko hilo ili kuleta uelewa kwa wadau wote wanaohusika.
Awali, akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri alisema kwa niaba ya serikali, ameafiki mapendekezo ya wajumbe na utayari wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela kutoa eneo katika jiji lake kwa ajili ya kufanyikia kwa mnada husika.
“Wazo mlilopendekeza la kuwa na kituo kimoja nchini cha kuuza dhahabu ni jema sana. Naliunga mkono. Sisi kama Serikali tutakuwa tukitangaza wanunuzi wakubwa waje kwenye mnada ili wanunue pale dhahabu. Tupunguze chaneli ya madalali hapa katikati ili kusudi mkutane na wanunuzi wakubwa uso kwa uso na kufanya biashara,” amebainisha Nyongo.
Mkuu wa Mkoa alimhakikishia Naibu Waziri na wadau wote kuwa ofisi yake ipo tayari kutoa eneo zuri na salama kwa ajili ya kuendeshea mnada husika.
Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa FEMATA, Bina aliwataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuzingatia haki na wajibu wao kama sheria na kanuni zinazoongoza sekta ya madini zinavyoelekeza ili kufanikisha maazimio ya mkutano huo kuhakikisha suala la utoroshaji madini linakoma.
“Sote tumekiri ukweli kwamba tunaiba, hatuchangii mapato, wengine hatujarasimishwa katika sekta, tujiulize tunafanya nini? Tumejipanga vipi? Lazima tulijue hilo,” amesisitiza.
Awali, akizungumzia lengo la kuandaa mkutano huo, Samamba alibainisha kuwa ni kutokana na changamoto ambayo imeibuka ya utoroshaji wa madini.
Kabla ya kufikia maazimio husika, asilimia kubwa ya wajumbe wa mkutano huo walikiri kuwa utoroshaji wa madini upo ambapo kwa madai yao, hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na utozwaji wa kodi na tozo mbalimbali stahiki.
Waliiomba serikali ipunguze kodi na tozo zilizopo ili waweze kumudu kuzilipa na hivyo kuachana na udanganyifu wa aina mbalimbali unaoendelea katika sekta hiyo.
Hata hivyo, akijibu hoja hiyo, Samamba alifafanua kuwa, suala la kulipa kodi limekuwa ni changamoto kwa wachimbaji wengi kutokana na kushindwa kutunza kumbukumbu zao, hivyo kulazimika kulipa zaidi tofauti na wale wanaomudu kutunza kumbukumbu ambao hujikuta wanalipa kodi kidogo.
Walitaja changamoto ya soko la uhakika linalosababishwa na wengi wao kutokufahamu bei halisi ya dhahabu na ndiyo sababu wengi wakapendekeza kuanzishwa kwa Soko la Pamoja.
Hivi karibuni, akiwa ziarani Geita, Naibu Waziri alipokea malalamiko kutoka kwa Mkuu wa Mkoa huo, Robert Luhumbi kuhusu utoroshaji wa madini ambapo aliahidi kuwa Serikali imedhamiria kwa dhati kuitafutia suluhisho changamoto husika.
Azma ya soko la pamoja inakuja wakati Serikali ikiwa imeshaamua kuwa na soko la pamoja katika madini ya tanzanite yanayochimbwa Tanzania pekee kote duniani.

No comments: