Wizara ya Mambo ya Nje yasisitiza hakuna maandamano Aprili 26
Kumekuwa
na taarifa kwenye mitandao ya kijamii zinazosambazwa na watu
wasioitakia mema nchi, zinazotishia usalama wa raia na mali zao. Taarifa
hizo zimewatia hofu baadhi ya raia wa kigeni na wanadiplomasia
wanaofanya kazi na kuishi hapa nchini.
Taarifa
hizo zimekuwa zikidai kuwa kutakuwa na maandamano yatakayofanyika
tarehe 26 Aprili 2018 na zinawaonya raia wa kigeni wasiende Zanzibar
katika kipindi cha Sikukuu ya Pasaka na sherehe za Muungano kwa sababu
za kiusalama.
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inawahakikishia
wanadiplomasia na raia wote wa kigeni wanaofanya kazi na kuishi nchini
na wananchi kwa ujumla kuwa, waendelee na shughuli zao ikiwemo kusafari
kutoka eneo moja kwenda jingine bila ya hofu yeyote kwa kuwa hakuna
dalili zozote za uvunjifu wa amani, usalama na utulivu wa nchi.Vyombo
vya usalama vipo makini vinatekeleza majukumu yake ipasavyo kuhakikisha
kuwa matukio yote ya uhalifu yanadhibitiwa kabla ya kuleta madhara kwa
umma.
Hivyo,
Wizara inawaomba wanadiplomasia, raia wa kigeni wanaoishi nchini na
wananchi kwa ujumla kuzipuuza taarifa hizo. Wananchi waendelee
kushirikiana kwa karibu na Serikali yao kupata taarifa sahihi kutoka
vyanzo vinavyoaminika badala ya kutegemea propaganda za watu wanaotumia
mitandao ya kijamii kwa maslahi binafsi.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 29 Machi 2018
No comments: