Ajali ya Basi Yaua Watano Kagera
Watu
watano wamekufa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya basi moja kati ya
manane yaliyokuwa yakisafirisha wakimbizi kutoka kambi ya Nduta
wilayani Kibondo mkoani Kigoma kuelekea nchini Burundi kupinduka.
Ajali hiyo imetokea leo Machi 29,2018 katika Kijiji cha Kasharazi wilayani Ngara mkoani Kagera saa 10:00 jioni.
Taarifa
zinasema ajali imetokea eneo la K9 lenye mteremko na kona kali baada ya
kupata hitilafu ya mfumo wa breki na kisha kuligonga lingine lililokuwa
mbele na baadaye kupinduka.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kagera, Agustino Olomi akizungumzia ajali hiyo
amesema miili ya waliofariki dunia bado haijatambuliwa pamoja na idadi
ya majeruhi.
Amesema
waliofariki dunia ni wanawake watatu na wanaume wawili. Kati yao yupo
mkazi wa Kasharazi aliyekuwa akiendesha baiskeli ambaye basi
lilimwangukia.
Mmoja kati ya madereva waliokuwa katika msafara huo, Raymond Revocatus amesema kila basi lilikuwa na wastani wa abiria 65.
Baadhi ya majeruhi wamepelekwa katika Hospitali ya Murugwanza wilayani Ngara kwa matibabu.
No comments: