Mbuzi wawili watoa uhai wa mtu
Hayo
yamebainishwa leo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna
wa Polisi Ahmed Msangi na kusema mbali na mtu huyo kuuwawa, Polisi
walifanikiwa kumuokoa Malecha Gilala (38) ambaye naye alikuwa
anashirikiliana na marehemu kufanya utapeli huo nyumbani kwa bwana
Lubeja Tulu, kwa kujifanya wao ni maofisa wa Polisi kuwa wamekwenda
kwake kwa lengo la kumkamata kutokana na mgogoro wa shamba uliopo kati
yake na jirani yake na kutaka wapatiwe kiasi cha fedha laki mbili ili
wasiweze kumpeleka Polisi.
Aidha, Kamanda Msangi amesema tukio hilo
limetokea jana (Aprili 04, 2018) majira ya saa 11:30 jioni katika
kijiji cha Nyanzumula kata ya Kagunga tarafa ya Nyanchenche wilaya ya
Sengerema mkoani Mwanza.
Inadaiwa kuwa kutokana na Lubeja
kutokuwa na fedha hizo aliwapa mbuzi wawili vijana hao ili wasiweze
kumkamata lakini kwa bahati mbaya matapeli hao walirudi siku nyingine
wakitaka wapatiwe tena ndipo Lubeja alipoamua kuenda kutoa taarifa kwa
mwenyekiti wa mtaa pamoja na Polisi lakini wakati askari walipokuwa
wanafanya ufuatiliaji wa kwenda eneo la tukio ghafla wananchi wenye
hasira kali waliwavamia na kuanza kuwashambulia matapeli hao na
kupelekea mmoja kufariki wakati alipokuwa akikimbizwa hospitalini
kutokana na kipigo alichokipata.
Kamanda Msangi amesema mpaka sasa hakuna
mtu yeyote aliyefanikiwa kukamatwa kuhusiana na tukio hilo, huku akitoa
onyo kwa wananchi kuacha tabia ya kutumia majina ya vyombo vya ulinzi
na usalama katika kufanya uhalifu.

No comments: