HOTUBA YA KAIMU MWENYEKITI WA JUKWAA LA WAHARIRI TANZANIA (TEF), DEODATUS BALILE KATIKA SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI DUNIANI (WPFD) ILIYOADHIMISHWA KITAIFA MEI 3, 2018 JIJINI DODOMA, TANZANIA
Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli,
Mhe. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe
Ndugu Mwenyekiti wa MISA-Tanzania, Salome Kitomari,
Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Kati Tanzania,
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Dk. Reginald Mengi,
Mwakilishi wa Jumuiya ya Ulaya,
Mwakilishi wa UNESCO, Anna Therese Ndong Jatta,
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), Fausta Musokwa,
Mkurugenzi Mkazi wa Friendrich-Ebert-Stiftung (FES), Andreas Quasten,
Rais wa UTPC, Deo Nsokolo
Mkurugenzi Mtendaji Tamwa, Edda Sanga
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mkajanga
Waandishi Wakongwe (wazee wetu tulionao hapa),
Waandishi wa Habari wote,
Mabibi na Mabwana
Mheshimiwa Rais, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kuendelea kutujalia uhai sote tulioko hapa, na ni kwa neema zake kuwa
leo tuko hapa kufanya shughuli hii muhimu ya kuimarisha ushirikiano kati
ya dola na vyombo vya habari kwa masilahi mapana ya maendeleo ya taifa
letu.
Nakushukuru kwa kukubali mwaliko wetu, kwani kwa kufanya
hivi Mhe. Rais umedhihirisha kwa matendo kauli yako uliyoitoa Bukoba
ulipozungumza na waandishi wa habari waliokuwapo katika ziara yako
kuwa “unawapenda waandishi wa habari, unawajali na unawathamini.”
Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari
Leo ni siku ya maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni Wajibu wa Uongozi: Vyombo vya Habari, Haki na
Utawala wa Sheria. Siku hii inaadhimishwa kidunia katika Jiji la Accra,
nchini Ghana. Kwa Tanzania, kitaifa inaadhimishwa hapa katika Jiji
jipya la Dodoma. Naomba kuchukua fursa hii kuwapongeza waandishi wa
habari wote nchini wanaofanya kazi hii ngumu ya kukusanya, kuchakata na
kuchapisha habari na taarifa kwa nia ya kuhabarisha, kuelimisha na
kuburudisha. Hongereni sana kuifikia siku hii muhimu katika historia ya
uandishi wa habari.
Kila Mei 3, waandishi wa habari duniani kote huadhimisha
siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari; Siku hii inaadhimishwa kwa nia ya
kupitia kiwango cha uhuru wa vyombo vya habari duniani, kulinda uhuru wa
vyombo vya habari na kutoa heshima kwa waandishi waliouawa wakiwa
kazini.
Mwaka 1993, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA)
ulipitisha azimio la Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani,
kutokana na Mapendekezo ya Mkutano wa 26 wa UNESCO uliofanyika mwaka
1991. UNESCO ilitoa maazimio hayo, baada ya Waadishi wa Magazeti barani
Afrika kuwa wamekutana jijini Windhoek, Namibia, mwaka 1991 na kutoa
azimio hili.
Hali ya Uhuru wa Habari nchini Tanzania
Mheshimiwa Rais, kabla ya Siku hii ya leo, Jukwaa la
Wahariri Tanzania (TEF) tumefanya mikutano miwili kujadili hali ya uhuru
wa vyombo vya habari Tanzania. Aprili 4, 2018 tulikutana jijini Dar es
Salaam ambapo tulikuwa na mjadala wa kina juu ya hali ya uhuru wa vyombo
vya habari na kisha tukatoa tamko la TEF. Kati ya Aprili 26 hadi 28,
mwaka huu Wahariri tumekutana Morogoro, ambapo nako tumepitia tena hali
ya uhuru wa vyombo vya habari Tanzania.
Kwa ujumla wake, Mhe. Rais tumebaini kuwapo hali ya
kuzorota kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini kutokana na matukio
machache tunayoyataja hapa chini kati ya mengi yaliyojitokeza ndani ya
mwaka huu wa kihabari tunaoumaliza.
1. Mhe. Rais, Mazingira ya kazi kwa Wanahabari yamekuwa
magumu kutokana na baadhi ya watendaji wa vyombo vya dola kuwabughudhi
na kufanya uonevu wa wazi dhidi yao wanapokuwa kazini (rejea matukio ya
polisi kuwanyanyasa waandishi wa habari wa Dar es Salaam, Mbeya, Iringa
na hapa Dodoma tulipo). Waandishi wamekuwa wakinyang’anywa simu zao,
kuwekwa chini ya ulinzi na kuachiwa bila kufikishwa mahakamani, hivyo
kuwatia wasiwasi wa kudumu.
2. Tukio la kupotea kwa mwandishi wa habari wa Gazeti
la Mwananchi, Azory Gwanda, aliyepotea Novemba 29, mwaka 2017 ambaye
hadi leo hajulikani alipo limeongeza hofu kwa waandishi wa habari hasa
wale wanaoripoti habari za uchunguzi.
3. Vyombo vya habari vinafanya kazi katika mazingira
magumu na ya woga kutokana na watendaji wake kuitwa na kuhojiwa na
mamlaka kama Idara ya Habari –Maelezo (kwa magazeti) na Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) (kwa vyombo vya kielektroniki) na wakati
mwingine kupewa adhabu kubwa za kulipa faini ama kufungiwa kama ambavyo
hivi karibuni vituo vya televisheni vya Star TV, ITV, Azam, EATV na
Channel 10 vimepigwa faini ya Sh milioni 65 na kuwekwa chini ya
uangalizi kwa kutangaza habari zilizotokana na press conference
iliyoitishwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa
kuvituhumu eti haviku-balance habari hiyo.
4. Hivi TCRA wanapotuita waandishi na kutueleza
mpangilio wa masafa au baadhi ya vituo kunyang’anywa masafa mbona huwa
tunatangaza habari hizo na hatupigwi faini kwa kuto – balance kwa
walionyanganywa masafa? Nchi yetu imefika huko kweli?
5. Mhe. Rais kuna kundi au watu wanaoitwawasiojulikana,
wameleta hofu kubwa miongoni mwa waandishi wa habari, kwa kiwango
ambacho katika historia ya nchi hii tumeshuhudia mwandishi Ansbert
Ngurumo akikimbilia nje ya nchi kwa maelezo kuwawatu
wasiojulikana walikuwa mbioni kuhatarisha maisha yake.
6. Tukio la kuzuia Bunge Live, ambalo lilianza rasmi
mwaka 2016 limeendelea kuwapo na kuwakosesha wananchi haki ya kupata
habari.
7. Mhe. Rais, Waziri Mwenye dhamana na masuala ya
habari, amekuwa akitumia vibaya kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za
Vyombo vya Habari kinachompa mamlaka ya kuzuia maudhui, lakini yeye
amekikitumia kwa nyakati tofauti kufungia magazeti kama Mawio,
Mwanahalisi, Mseto, Tanzania Daima and Raia Mwema.
8. Kifungu hiki cha 59 kinasema: “The Minister shall
have powers to prohibit or otherwise sanction the publication of any
content that jeopardizes national security or public safety. Mantiki na
msisitizo wa kifungu hiki upo kwenye maudhui (content) na si gazeti
lililochapisha.
9. Mhe. Rais, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
kupitia kwa Waziri Mwenye dhamana na masuala ya habari imetunga kanuni
za kudhibiti mitandao ya kijamii za mwaka 2018 ambazo kiuhalisia
hazitekelezeki. Zinatoa majukumu na wajibu, ambavyo ni vya kikampuni kwa
mtu ambaye anaanzisha blog kuwasiliana na ndugu na jamaa, jambo
linalokiuka haki za msingi za binadamu.
10. Yamekuwapo matukio ya watendaji wakuu wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi kuviandama vyombo vya habari vinavyofanya kazi ya
kuonyesha kinachoendelea nyakati za uchaguzi (kwa mfano kuibwa na
kurejeshwa kwa sanduku la kura pale Kinondoni), waandishi kuitwa na
kuhojiwa bungeni na mengine mengi.
Mhe. Rais, hali inayoendelea nchini na baadhi ya matukio
niliyoyataja, hayana afya kwa taifa letu huko tuendako. Tunayo mifano ya
nchi nyingi duniani,zikiwamo zile ambazo ni majirani zetu, ambazo
ziliingia katika gharama kubwa ya watu wake kwa kudharau matukio madogo
madogo kama ambayo yanatokea nchini mwetu hivi sasa.
Sisi waandishi wa habari, tukiwa wataalamu wa habari,
tunaowatangulia wenzetu kuona kinachotokea kwa jicho la kiuchambuzi,
narejea wito wa kuwapo kwa mjadala wa kitaifa kuhusu mustakabali wa
uhuru wa habari nchini, ambao hatima yake ni amani na maridhiano ya
kitaifa, kwa kushirikisha wadau wengine wa habari, kabla hayajatukuta
makubwa yaliyowakuta wenzetu. Tujifunze kwa wenzetu kwamba vyombo vya
dola vinaweza kufanya kazi yake vizuri vikiwa vinaungwa mkono na raia wa
taifa husika, bila kuviburuza vyombo vya habari.
Mwisho, si kwa umuhimu Mhe. Rais, natambua na kupongeza
juhudi za serikali za kusimamia misingi ya uwajibikaji, vita dhidi ya
rushwa na ufisadi, usimamizi wa mapato ya serikali, matumizi endelevu ya
rasilimali za umma (hasa sekta ya madini), ujenzi wa miundombinu kama
vile reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge, mradi mkubwa wa umeme
wa Stiegler’s Gorge, uimarishaji wa shirika la ndege (ATCL), kuhamia
makao makuu Dodoma, usimamizi wa Sera ya Viwanda na mengine kadha wa
kadha, ambayo ni vyanzo vya habari tunazozichapisha.
Hata hivyo, tunasisitiza kuwa maendeleo haya yatakuwa na
maana zaidi kwa kuwa na taifa ambalo wananchi wake wanaishi kwa amani
halisi na kuaminiana, bila kuogopa watu wasiojulikana.
Asanteni kwa kunisikiliza.

No comments: