Mtanzania auawa kwa kugongwa na gari kwa makusudi Afrika kusini.
WIZARA
ya Mambo na Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imethibitisha kifo
cha mwanafunzi Mtanzania aliyekuwa akisoma nchini Afrika Kusini.
Msemaji
wa Wizara hiyo, Mindi Kasiga alifafanua kuwa kwa sasa wizara
imewasiliana na Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini ili kubaini
undani wa suala hilo.
Alisema
wizara bado haina taarifa za kina kuhusiana na suala hilo na kuwa
inafuatilia kujua chuo alichokuwa akisoma, siku ya tukio hilo na masuala
yote muhimu kuhusiana na kifo hicho.
Jana
kulikuwa na taarifa iliyokuwa ikizunguka kwenye mitandao ya kijamii
ikielezea kuwa kuna Mtanzania ameuawa kikatili nchini Afrika Kusini.
Taarifa
hizo zilidai kuwa mwanafunzi aliyejulikana kwa jina la Baraka Nafari
aliyekuwa akichukua Shahada ya Uzamivu (PHD) katika Chuo Kikuu cha
Johannesburg (UJ) aliuawa mapema Ijumaa Februari 23, mwaka huu kwa
kugongwa na gari mara mbili na kubamizwa kwenye ukuta na baadaye
kushambuliwa kwa visu.
Ziliendelea
kudai kuwa kamera za usalama za CCTV za chuo hicho zilionesha Baraka na
mwanafunzi mwenzake wakikimbia kujiokoa wakati wanaume wawili kwenye
teksi wakiwaandama.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo kamera hiyo iliendelea kumuonesha dereva wa
teksi akimgonga kwa makusudi mwanafunzi huyo kwenye uzio wa makazi ya
chuo hicho yaliyoko Auckland Park na kumuua.
Taarifa
hizo ziliendelea kusema kuwa dereva wa gari hilo alikamatwa na polisi
kwa kuendesha bila leseni, lakini baadaye aliachiwa huru bila
kufunguliwa mashtaka yoyote.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo, zinazoonekana kuandikwa na wafanyakazi na
wanafunzi wa chuo hicho wakitaka polisi na uongozi wa chuo kuchukua
hatua dhidi ya mauaji ya mwanafunzi huyo waliomuelezea kuwa alikuwa
akipendwa na wafanyakazi na marafiki wa Chuo hicho na kuwa hawataacha
maswali kuhusu mazingira ya kuuawa kwake bila kupata majibu.

No comments: