Serikali yataka madini ya Nickel yaongezwe thamani
Naibu
Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amesema kuwa Serikali itaboresha
mazingira ya uwekezaji wa Madini ya Nickel yanayopatikana Ngara mkoani
Kagera lakini pia itahakikisha wawekezaji wanayaongezea thamani Madini
hayo hapa nchini kabla ya kuyasafirisha nje ya nchi ili kuleta tija
zaidi.
Aliyasema
hayo Machi Mosi alipotembelea Mradi wa Uwekezaji wa Madini ya Nickel
wa Kabanga, uliopo wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera, akiwa katika ziara ya
kazi.
“Sisi
kama Serikali tutahakikisha tunawaletea wawekezaji miundombinu ya
Barabara, Reli na Umeme ili kuwajengea mazingira rafiki ya uzalishaji
lakini kwa upande wao tunataka kuona uwekezaji makini; wachimbe na
kuongeza thamani ya madini hayo hapa nchini. Badala ya kutoa Nickel kama
malighafi, watoe bidhaa zinazotokana na Nickel.” alisema Nyongo.
Alisema
kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha Madini hayo muhimu, ambayo kwa
sasa Soko lake Duniani limeanza kupanda, yanalinufaisha Taifa kwa
kiwango kinachostahili.
Akifafanua,
Naibu Waziri alisema kuwa, Nickel ikiongezewa thamani hapa nchini,
miundombinu ya Reli, Umeme na Barabara ikaboreshwa; kutakuwa na uhakika
wa kuuza Madini hayo kwa bei nzuri na kuleta ushindani kwenye Soko la
Dunia.
“Tunataka wawekezaji wachimbe ili tupate kodi, tupate mrabaha lakini pia wananchi wa maeneo haya waweze kupata ajira.” alisema.
Akijibu
swali kutoka kwa mmoja wa waandishi wa habari walioshiriki katika ziara
hiyo, ambaye alitaka kujua Serikali ina mtazamo gani kuhusu umakini wa
mwekezaji aliyepo sasa, Naibu Waziri alisema kuwa Serikali inamchukulia
mwekezaji huyo kama mwekezaji makini kutokana na namna alivyojipambanua
katika shughuli hiyo.
“Mtu
ambaye amewekeza kiasi cha Dola Milioni 275 hadi kufikia sasa, sioni
kwamba anatania katika uwekezaji. Namwona ni mwekezaji aliyedhamiria na
aliye makini.” alisema.
Hata
hivyo, Nyongo alibainisha kuwa Serikali itaendelea kukaribisha
wawekezaji wengine makini katika sekta hiyo ili kwa pamoja wasaidie
kuinua Pato la Taifa kupitia uwekezaji wao.
Awali,
akiwasilisha Taarifa ya utendaji kazi wa Mradi wa Kabanga Nickel,
Meneja Mkazi wa Mradi huo, Andrew Msola alimweleza Naibu Waziri kuwa
changamoto kubwa waliyonayo ni ukosefu wa miundombinu muhimu ya
Barabara, Reli pamoja na Umeme; ambapo Naibu Waziri aliahidi Serikali
kushughulikia suala hilo kwa haraka.
Ilielezwa
kuwa Mradi wa Kabanga Nickel ulianza uzalishaji wa Madini ya Nickel
zaidi ya miaka 40 iliyopita, lakini tangu mwaka 2009 ilisimamisha
uzalishaji kutokana na kuporomoka kwa bei ya Madini hayo katika Soko la
Dunia.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Naibu Waziri aliwaeleza kuwa, kwa sasa Soko la
Madini hayo limeanza kuimarika kutokana na kukua kwa teknolojia ambayo
imesababisha kuongezeka kwa matumizi ya Madini ya Nickel ikiwemo
kutumika katika Magari ya Umeme badala ya yale yanayotumia mafuta.
“Mathalani
Miji mikubwa ya Ulaya hivi sasa, wanataka waachane na Magari
yanayotumia mafuta na kujikita kwenye yale yanayotumia Betri
zinazochajiwa kwa umeme. Aidha, Dunia nzima sasa inazungumzia suala la
utunzaji wa mazingira, hivyo kila mmoja anataka kuachana au kupunguza
matumizi ya mafuta ili kutunza mazingira.”
Baada
ya Kagera, Naibu Waziri ameelekea Mkoa wa Kigoma ambako anatarajia
kuhitimisha ziara yake. Awali, katika ziara hiyo, alitembelea Mikoa ya
Mwanza na Geita.

No comments: