Mwanajeshi Anayedaiwa kuua askari mwenzake apandishwa kizimbani
Mwanajeshi
MT 109795 Private Ramadhan Mlaku (28) amefikishwa Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu akikabiliwa na shitaka la mauaji ya askari mwenzie, MT
79512 SGT Saimon Munyama.
Mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo leo Jumatano Machi 14, 2018 saa tano asubuhi na gari la kubebea wagonjwa.
Alishushwa
katika gari hilo akiwa juu ya kitanda cha wagonjwa na kupelekwa chumba
cha mawakili wa Serikali ambapo alisomewa shtaka linalomkabili.
Akisomewa
shtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakili wa Serikali,
Mosii Kaima amesema mtuhumiwa huyo anadaiwa kufanya kosa hilo Oktoba 30,
2017.
Imedai
kuwa mshtakiwa ambaye ni mwanajeshi wa kambi ya Jeshi Makongo siku hiyo
akiwa Makao Mkuu ya JWTZ Upanga, Dar es Salaam alimuua askari mwenzie
MT 79512 SGT Munyama.
Baada
ya kusomewa shtaka hilo, mshtakiwa huyo hakuruhusiwa kuongea chochote
kwa sababu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza
kesi hiyo.
Pia kosa hilo hakuna dhamana kwa mujibu wa sheria.
Upande
wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na Hakimu Simba
aliutaka upande wa mashtaka kujitahidi kukamilisha upelelezi wa kesi
hiyo mapema.
Kesi imeahirishwa hadi Machi 28, 2018 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.
Baada ya kusomewa shtaka hilo mshtakiwa huyo alipandishwa tena katika gari la wagonjwa na kurudishwa mahabusu.
No comments: