Header Ads

Hatuwezi kuyavumilia haya- Waziri Mwigulu




Serikali ya awamu ya tano kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema haiwezi kuvumilia kuona wananchi wake wanapata shida, wanaumizana kutokana na matukio ya uchaguzi kisha wao wakae kimya bila ya kuchukua maamuzi yeyote kwa kuwa wao wapo kwaajili ya kulinda usalama wao.
 
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa wizara hiyo Mwigulu Nchemba leo (Aprili 10, 2018) kwenye mkutano wa 11 kikao cha sita kinachoendelea kufanyika mkoani Dodoma wakati akitoa maelezo ya jumla kwa baadhi ya hoja zilizotolewa na Wabunge katika kikao cha Bunge cha 11 zilizoelekezwa katika Wizara yake.

"Sisi kama Jeshi la Polisi na kama Wizara ya Mambo ya Ndani hatupendi kuona wananchi wetu wanaumizana kwenye masuala ya uchaguzi na kwenye chaguzi nyingi tumeshuhudia. Mara zote huwa nasema kwamba ni aibu sana kwa nchi yenye vyama vingi vya siasa halafu wananchi wake wanafanyiana fujo pale panapotokea uchaguzi katika eneo husika", amesema Waziri Mwigulu.
Pamoja na hayo, Waziri Mwigulu ameendelea kwa kusema "tulitarajia watu waheshimu taratibu kwa maana wakifanya hivyo hapata kuwepo na ugomvi katika maeneo husika. Lakini sisi kama Wizara ya Mambo ya Ndani hatutavumilia kuona kwamba watu wanakatana mapanga halafu tukasema ni kwasababu ya uchaguzi ama ni siasa tukayaacha hilo hatuwezi, sisi tunawajibika kulinda usalama wa raia mara zote pale inapotokea mikusanyiko katika maisha yao ya kawaida".
Mbali na hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amewataka Wabunge waliopo Bungeni humo kuacha tabia ya kuunganisha matukio na imani ya dini au siasa.
"Niwaombe Wabunge wenzangu, pale inapotokea tatizo linalompata mmoja wa watanzania tuepuke sana kuliunganisha jambo hilo na dini yake kwa sababu yanapotokea mambo ya kihalifu mtu akamatwi kutokana na dini, kabila wala chama chake cha siasa alichopo. Mtu anakamatwa kutokana na kosa alilofanya kwa hiyo tusije tukatumia utaratibu wa kuunganisha kosa alilofanya na dini, kabila au chama chake cha siasa", amesisitiza Mwigulu

No comments:

Powered by Blogger.