Taarifa Toka Ofisi ya Waziri Mkuu Baada ya Kuzindua Mbio za Mwenge
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa mikoa ya Tabora, Geita,
Mtwara na Shinyanga ambayo inaongoza kwa utoro wa wanafunzi kwa shule za
sekondari wahamasishe umuhimu wa elimu na mahudhurio endelevu shuleni.
“Kwa
ujumla utoro wa wanafunzi wa Sekondari ni mkubwa zaidi kwa Mikoa husika
kuliko shule za msingi. Nitumie nafasi hii kuikumbusha Mikoa
niliyoitaja kuhamasisha wananchi wakiwemo wazazi, walezi na wanafunzi
wenyewe kuhusu umuhimu wa elimu na mahudhurio shuleni.”
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Aprili 02, 2018) wakati akizindua
mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2018 katika uwanja wa Magogo mkoani
Geita. Kaulimbiu ya mbio za mwenge kwa mwaka huu ni ‘Elimu ni ufunguo wa
maisha, wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa letu.’
Waziri
Mkuu amesema dhamira ya Serikali kupitia kaulimbiu hiyo ni
kuwashirikisha wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo kuwekeza katika
elimu na kuzalisha rasilimali watu yenye ujuzi na stadi zitakazowezesha
kuchochea mapinduzi ya viwanda ili nchi iwe ya uchumi wa kati ifikapo
2025.
Akizungumzia
kuhusu utoro kwa shule za sekondari nchini, Waziri Mkuu amesema mkoa wa
Tabora ndio unaongoza kwa utoro kwa kuwa na silimia 9.7,
Geita asilimia 8.1, Mtwara asilimia 6.4 na Shinyanga asilimia 6.3.
Kuhusu
utoro wa wanafunzi wa shule za Msingi nchini, Waziri Mkuu amesema mkoa
unaoongoza ni wa Rukwa kwa asilimia 3.2, Geita asilimia 3.1, Tabora
asilimia 2.9, Simiyu asilimia 2.0 na Singida asilimia1.9.
Amesema
mikoa yenye kiwango kikubwa cha utoro wa wanafunzi na kuacha shule
ihakikishe mahudhurio yanadhibitiwa shuleni ili kuhakikisha wanafunzi
wote wanaoandikishwa wanahudhuria, wanasoma na kuhitimu ngazi husika.
“Ukitaka
kuleta maendeleo ya uchumi ulio imara, ukitaka kujenga jamii inayo
heshimu na kufuata misingi ya uwajibikaji na ubunifu, ukitaka kujenga
Taifa lenye amani na utulivu, lazima uwekeze zaidi katika elimu”.
“Kwa
hiyo, uwekezaji katika elimu haumaanishi tu kuhakikisha watoto wetu na
Watanzania kwa jumla wanapata haki yao ya msingi bali ni kuweka misingi
imara itakayo liwezesha Taifa na mtu binafsi kufikia hatua bora ya
maisha”.
Waziri
Mkuu amesema ili kuhakikisha Taifa linafikia viwango bora vya elimu,
Serikali ya awamu ya tano inyoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli,
imedhamilia kuboresha elimu katika ngazi zote nchini, kuanzia Elimu ya
Awali hadi Elimu ya Juu.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka
huu zitaendelea kuhimiza mapambano dhidi ya rushwa kwa sababu bado ipo
na inaendelea kuwa ni adui wa haki na kudhoofisha jitihada za Serikali
za kuimarisha uchumi, kuimarisha huduma za jamii na Utawala bora.
Amesema
athari zinazotokana na vitendo vya rushwa huwaathiri watu wa kawaida
zaidi na kuendelea kubaki wanyonge katika jamii, hivyo Serikali
itaendelea kupambana na vitendo vya rushwa bila kuchoka mpaka jamii
itakapoachana na vitendo hivyo vya kidhalimu.
Awali,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira
na Wenye Ulemavu Bibi Jenista Mhagama alisema Mwenge wa Uhuru
utakimbizwa umbali wa takribani kilomita 103,440.7 kwa siku 195 katika
mikoa yote 31 nchini na halmashauri za wilaya 195.
Alisema
kazi hiyo itafanywa na vijana sita kutoka Tanzania Bara na Zanzibar
ambao wameandaliwa kikamilifu ili kuhakikisha wanaendelea kuwakumbusha
Watanzania historia ya falsafa ya Mwenge wa Uhuru, kufikisha kwa ufasaha
ujumbe wa mwaka huu na kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo kwa
umakini.
Bibi
Jenista alisema mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 zinaongozwa na Bw.
Charles Kabeho kutoka mkoa wa Dar es Salaam akishirikiana na Bw. Issa
Abasi Mohamed (Kusini Pemba), Bi. Agusta Safari (Geita), Bw. Ipyana
Mlilo (Tanga), Bw. Dominick Njunwa (Kigoma) na Bi. Riziki Hassan Ali
(Kusini Unguja).
Naye,
Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo - Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar Balozi Ali Abeid Karume alisema atahakikisha ujumbe wa Mwenge
wa Uhuru unawafikia wananchi wote pamoja na kupita katika miradi yote ya
maendeleo iliyopangwa.
Balozi
Karume ametumia fursa hiyo kuwapongeza Rais Dkt. Magufuli pamoja na
Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Shein kwa jitihada zao za kudumisha
amani, utulivu, kuwaletea wananchi maendeleo bila ya ubaguzi pamoja na
kupambana na maadui wanaotaka kudhoofisha maendeleo nchini.
No comments: