Tanzania Yapata Mkopo Wa Shilingi Bilioni 34 Kutoka Mfuko Wa Maendeleo Wa Abu Dhabi Kuboresha Barabara Ya Uvinza-malagarasi Kwa Kiwango Cha Lami
Benny Mwaipaja, Abu Dhabi
Tanzania
imeendelea kuaminiwa na Jumuiya ya Kimataifa ambapo Mfuko wa Maendeleo
wa Umoja wa Falme za Kiarabu-Abu Dhabi, umeipatia Tanzania mkopo wenye
masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 15, sawa na shilingi bilioni
34 za Tanzania, kwa ajili ya kuboresha barabara ya Uvinza hadi
Malagarasi yenye urefu wa kilometa 51, kwa kiwango cha lami
Hafla
fupi ya uwekaji saini wa mkataba huo imefanyika katika makao makuu ya
Mfuko huo yaliyopo Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ambapo
Mhandisi Mussa Ibrahim Iyombe, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI, amesaini kwa niaba ya Serikali, na
Mhe. Mohamed Saif Al Suwaidi Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa
Abu Dhabi kwa niaba ya Mfuko huo.
Akizungumza
baada ya kusaini Mkataba huo, Katibu Mkuu-TAMISEMI, Mhandisi Mussa
Iyombe, amesema kuwa barabara hiyo ni muhimu kwa kuwa ni kiungo kikuu
cha usafiri wa abiria na mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda
Kigoma na nchi jirani za Burundi na Kongo DRC.
Amesema
kuwa uamuzi wa Serikali wa kuboresha barabara hiyo kwa kiwango cha lami
umelenga kuchochea uchumi wa nchi kwa kuwezesha usafirishaji wa mazao
ya wakulima pamoja na kupunguza gharama na kuongeza uwezo wa kufanya
biashara na nchi hizo jirani.
“Tutabakiwa
na kipande cha barabara yenye urefu wa kilometa 28 kutoka Urambo hadi
Kaliua na kilometa 42 kutoka Chagu hadi Kazilambwa, barabara ambazo
Serikali inaendelea kuzitafutia fedha ili kukamilisha barabara yote
inayoelekea ukanda huo wa kati kutokea Dar es Salaam, Manyoni (Singida),
Tabora hadi Kigoma” Alisema Mhandisi Iyombe.
Ameushukuru
Mfuko huo kwa kuendelea kuiamini Serikali na kutoa mkopo huo wenye
masharti nafuu baada ya kufanya hivyo hivi karibuni kwa kutoa mkopo
mwingine wa dola milioni 57, uliofanikisha kuboreshwa kwa barabara ya
Kidahwe hadi Uvinza yenye urefu wa kilometa 77 kwa kiwango cha lami.
Mkurugenzi
Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi, Mhe. Mohamed Saif Al Suwaidi,
kwa upande wake, amesema kuwa Mfuko huo uko tayari kushirikiana na
Serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo
nchini.
Amefafanua
kuwa mradi huo ambao mkataba umesainiwa mjini Abu Dhabi, utakuwa ni wa
nne kufadhiliwa na Mfuko wake Tangu uhusiano wa Umoja wa Falme za
Kiarabu (UAE) na Tanzania uanzishwe mwaka 1977, ukiwemo mradi wa
kuendeleza kiwanda cha Sukari cha Kagera, Mradi wa Maji Vijijini huko
Viwani Zanzibar na Mradi wa kuboresha barabara ya Kidahwe hadi Uvinza
kwa kiwango cha lami.
Kwa
upande wake, Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE)
Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk amesema kuwa kusainiwa kwa mkataba huo ni
kiashiria cha kukubalika kwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na
Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, katika kuwaletea wananchi wake
maendeleo ya haraka na kuungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa.
“Hatua
hii ni uthibitisho wa mahuasiano mazuri ya kihistoria na kidugu kati ya
Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu uliodumu kwa muda mrefu tangu
mwaka 1977” Alisisitiza Mhe.Mbarouk
Mhe.
Mbarouk amebainisha kuwa kukamilika kwa barabara hiyo ya Uvinza hadi
Malagarasi kutachochea maendeleo ya kiuchumi na mapinduzi ya viwanda kwa
kuunganisha shughuli za kiuchumi kama vile kilimo na maliasili pamoja
na kukuza utalii.
No comments: