Wabunge wa kambi ya Upinzani kutoka Zanzibar watoka nje ya Bunge wakishinikiza Muungano ujadiliwe
Wabunge
wa Chama cha Wananchi (CUF) Zanzibar, leo walitoka kwenye ukumbi wa
Bunge baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan ‘Zungu’ kusitisha
kujadili masuala yanayohusu muungano.
Hatua
hiyo ya Zungu imetokana na mwongozo ulioombwa na Waziri wa nchi Ofisi
ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu,
Jenista Mhagama, ambaye alisema lugha zinazotumiwa katika mjadala wa
suala hilo, unafanya Serikali ionekane kuwa haijali muungano.
Baada
ya kauli hiyo Zungu alitangaza kusitisha mjadala wa Muungano, jambo
lililofanya baadhi ya wabunge kusimama wakiomba mwongozo kutaka kujua ni
kwa namna gani amesitisha hoja hiyo wakati iko kwenye Hotuba ya Waziri
Mkuu inayotarajiwa.
Baada
ya kutoka nje ya Bunge, Mbunge wa Mji Mkongwe, Ali Saleh amesema
wameamua kutoka kwasababu ya kukatazwa kujadili mambo ya Zanzibar ambayo
ndiyo wanayoyatetea ndani ya Bunge.
“Kama
hawataki tujadili mambo ya Zanzibar tukae tufanye nini tena, leo
tumetoka wenyewe lakini wakiendelea hivi watatufanya tutoke na watu
wajue ni kwanini tumetoka na hapo watakuwa wamehatarisha Muungano,”
amesema Saleh.
Mapema
jana, suala hilo liliibuka likianzia kwa Mbunge wa Viti Maalumu Mariam
Msabaha (Chadema), akizungumzia kuwa serikali ya Muungano inaiminya
Zanzibar na kushindwa kujitangaza kimataifa.
Hoja
hiyo iliendelea kwa wabunge kuendelea kuchangia na kuomba miongozo
lakini alipoanza kuchangia Mbunge wa Tunduru Frank Mwakajoka (Chadema)
ambaye alitangaza kuwa wabuge wa chama tawala wanaiumiza Zanzibar na nia
yao siyo njema kuhusu muungano.
Kauli
ya mbunge huyo ilimuibua Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Kangi
Lugola ambaye aliomba mwongozo na kuwataka wabunge kumtaja mbunge ambaye
anapinga Muungano vinginevyo wasitoe kauli hizo.

No comments: