Familia Yaendelea Kupiginia Haki za Tundu Lissu
Familia
ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), imesema haki
anazostahili ndugu yao zikiwamo gharama za matibabu, uchunguzi wa
waliomshambulia kwa risasi, zitacheleweshwa kwa muda lakini hatimaye ipo
siku atazipata.
Msemaji
wa familia hiyo, Wakili Alute Mughwai, alisema hayo jana wakati
akizungumza na wanahabari ofisini kwake, jijini hapa.Alisema familia
haitachoka kudai haki za Lissu na kinachojitokeza ni kucheleweshwa
lakini siku moja itapatikana.
Akizungumzia
haki ya kupata matibabu, alinukuu kifungu cha 24 cha Sheria ya Utawala
wa Bunge, 2008, kinachotoa haki hiyo kwake na mwenza wake pamoja na
watoto wanne na kwamba utaratibu mwingine wowote unaokwenda kinyume
unakiuka sheria hiyo.
“Mbunge
si mtumishi wa serikali, mbunge ana taratibu zake za kupata matibabu…
Bunge kama mhimili unaojitegemea hauna taratibu zingine zaidi nje ya
sheria hiyo,” alisema.
Aprili
19, mwaka huu, Spika wa Bunge Job Ndugai, aliliambia bunge
linaloendelea mjini Dodoma kuwa, familia ya Lissu haijawasilisha Ofisi
ya Bunge nyaraka muhimu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Wizara ya
Afya Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Ofisi ya Rais.
Alisema
iwapo nyaraka hizo zitapatikana, ofisi yake haitasita kuidhinisha
malipo ya matibabu yake.Hata hivyo, Wakili Mughwai alisema utaratibu huo
haupo katika sheria ya Bunge.
“Unaposema
fuata utaratibu wakati mbunge amepigwa risasi na yupo katika hatari ya
kufa unataka kupata nini zaidi? Bunge ambalo ni mhimili unaojitegema
limekuwa na utaratibu wa kushughulikia mbunge aliye katika hatari ya
kufa baada ya kupigwa rasasi?,” alihoji.
“Huo utaratibu haupo…ni lazima ubuniwe utaratibu wa kuendana na hayo mazingira.”
Alisema
tangu kushambuliwa kwa Lissu Septemba 7, mwaka jana mjini Dodoma,
familia imekuwa na mawasiliano ya muda mrefu na Ofisi ya Bunge kuhusu
matibabu ya Lissu, lakini hata mara moja hawajasema wazi kuhusu
utaratibu.
“Kama
Bunge wangesema tangu mwanzo katika majadiliano yao kuwa hawawezi
kugharimia matibabu yake, tungewaambia ‘thank you’ na kusingekuwapo na
vikao vya mjadala,” alisema.
Alisema
kwa mfano, Februari 1, mwaka huu, walipokea barua ya Bunge iliyowaarifu
kuwa wanawasiliana na Wizara ya Afya kuhusu matibabu ya Lissu na
baadaye watawaarifu.
“Ni
miezi mitatu sasa, Mei 2 familia imeandika barua Ofisi ya Bunge kuomba
mrejesho huo na kujua wamefikia wapi,” alisema. Akizungumzia upelelezi
wa tukio hilo, Wakili Mughwai alisema miezi minane sasa imepita na wao
bado wanapata kiza kikuu.
“Alishambuliwa
kwa risasi na watu wasiojulikana miezi minane iliyopita na walitakiwa
kufanya upelelezi wa kuwatia hatiani watuhumiwa,” alisema huku
akisisitiza kuwa wataendelea kudai haki ya ndugu yao bungeni na haki
kama mwathirika wa kosa la kijinai.
“Tutaendelea kudai haki hizi hadi zitakapopatikana. Tunajua haki ya mtu inacheleweshwa lakini haitapotea,” alisema.
Akizungumzia hali yake alisema anatarajiwa kufanyiwa operesheni ya 20 ya kurekebisha mifupa katika paja la kulia.
Alisema
operesheni iliyopita ilifanyika vizuri na sasa yupo kwa uangalizi wa
madaktari kwa siku chache zijazo na baada ya hapo ataendelea na mazoezi
ya viungo.
Alisema
pamoja na operesheni hiyo atafanyiwa operesheni nyingine ndogo kufuatia
kuambukizwa vijidudu na pia kunyoosha mfupa katika paja.
Kuhusu kurudi nchini, alisema hata yeye hajui na kama familia pia haijui.
“Wengi
wanatuuliza lini atakuja, jibu letu ni hatujui, na sisi ni watu wa
kwanza kutaka arudi nyumbani…hilo ni suala la madaktari wanaomtibu.
“Lissu si mtoto mdogo, anahitaji kutibiwa hayo majeraha na akishapona anatamani kurudi nyumbani,” alisema.
Aikana Kauli ya Spika
Wakili
Mughwai alikanusha taarifa ya Spika wa Bunge Ndugai aliyedai kuwa
gharama za matibabu ya Lissu yanalipwa na Serikali ya Ujerumani.
“Hiyo
habari si ya kweli,” alisema huku akiweka bayana kwamba matibabu ya
Lissu, weka na posho za kujikimu vinagharimiwa na wasamaria wema.
“Hii habari imetufedhehesha sana kwa namna moja inatuonyesha sisi familia kuwa ni matapeli.
“Athari ya hii taarifa ni kuwaambia watu waliokuwa wanamchangia gharama za matibabu yake waache,” alisema.
Alisema
familia wangekuwa watu wa kwanza kabisa kushukuru kwa kumpata mfadhili
huyo mkubwa na wangewaomba wananchi waache kumchangia. Alisema Lissu
bado yupo hospitalini na anahitaji msaada.
Wakili Mugwai alitoa namba ya akaunti ya Lissu ya CRDB ambayo ni 01J2043045300 yenye jina la Tundu Antiphas Lissu.

No comments: